''Mzozo wa Somalia ni wa kimataifa''

Kijana mdogo akiongoza wapiganaji wa Al shabab
Image caption Kijana mdogo akiongoza wapiganaji wa Al shabab

Waziri mpya wa usalama nchini Somalia, amesema vita nchini humo sio mzozo wa wenyewe kwa wenyewe, lakini ni mzozo wa kimataifa.

Waziri huyo Ahmed Abdisalam, amewaambia waandishi wa habari jijini Nairobi kuwa Somalia inashambuliwa na wapiganaji wa kigeni wenye uhusiano wa karibu na wanamgambo wa Al Qaeda.

Amesema jamii ya kimataifa, inapaswa kuunga mkono juhudi za kumaliza vita nchini humo.

Majeshi ya Umoja wa Afrika yamekuwa nchini Somalia kwa miaka miwili sasa, ili kuisaidia serikali ya mpito ambayo inapigana na wanamgambo wa Al Shaabab na washirika wao.

Image caption Ndugu wakimbeba mwenzao baada ya shambulio Somalia

Waziri huyo wa usalama wa Somalia, amesema shambulio la hivi karibuni dhidi ya mashabiki waliokuwa wakitazama fainali ya kombe la dunia mjini Kampala, limeonyesha ukweli wa hali yenyewe, kuwa vita nchini Somalia vinahusu jamii ya kimataifa.

Amesema mzozo huo unahitaji suluhisho la haraka. Majeshi ya Umoja wa Afrika yanayohudumu nchini Somalia ni kutoka nchi za Uganda na Burundi pekee.

Mzozo huo wa Somalia utakuwa katika ajenda ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika utakaoanza mjini Kampala hapo Jumapili.

Hatahivyo haijabainika kama viongozi wa Umoja wa Afrika wana nia ya kupeleka majeshi yao nchini Somalia.