Waasi Darfur kutotumia askari watoto

Image caption Waasi wa kundi la Jem

Kundi moja la waasi la Sudan linatarajiwa kutia saini mkataba wa kuruhusu Umoja wa Mataifa kuingia kwenye makao yao kuhakikisha kuwa hakuna watoto walioajiriwa kama askari.

Kundi la the Justice and Equality Movement Jem, limeiambia BBC limekuwa likijaribu kuwalinda watoto tangu kuanza kwa mgogoro wa Darfur wa miaka saba.

Umoja huo umesema watoto waliokutwa kwenye maeneo ya jeshi au waliopo kwenye maeneo yenye migogoro wanaweza kuondolewa kutokana na makubaliano hayo.

Takriban watoto 6,000 wamejikuta wakiwa maaskari kwenye mgogoro huo wa Darfur.

Mwandishi wa BBC Imogen Foulkes mjini Geneva amesema shirika linaloshughulikia watoto la Umoja wa Mataifa limefurahia makubaliano hayo, yaliyochukua zaidi ya mwaka kuafikiana, na ni maamuzi muhimu huku wakiwa na matumaini kuwa makundi mengine ya waasi yatafuata.

Viongozi wa kundi hilo la Jem, waliosafiri kuelekea Geneva kwa ajili ya kutia saini mkataba huo, wamesema hawana maaskari watoto lakini walikuwa wakitia saini kama nia ya kuonyesha kuridhia makubaliano hayo.

Mapigano yaliongezeka mjini Darfur mwezi Mei baada ya Jem kujitoa katika mazungumzo ya amani na serikali, likidai kuwa serikali haikuwa na nia safi.

Mapigano baina ya waasi na wapigananji wanaoungwa mkono na serikali magharibi mwa Sudan yanakadiriwa na umoja wa mataifa kusababisha vifo vya watu 300,000 na watu milioni 2.7 kukimbia makazi yao.