Wateja milioni 500 wa facebook

Image caption Mwanzilishi wa facebook

80% ya idadi yote ya watu duniani sasa hivi wana kurasa kwenye tovuti ya face book. Tovuti hii ilioanzishwa miaka sita iliopita na mwanafunzi mmoja kutoka chuo kikuu cha Harvard nchini Marekani imebadilisha utaratibu mzima wa jinsi watu wanavyowasiliana.

Lakini licha ya kuwa mwanzilishi wa tovuti hiyo Mark Zuckerberg ana sifa za billionaire, huduma hiyo inatumika bure na kipato chake kutoka matangazo ya biashara kidogo sana. Mwaka huu, kiwango hicho kilikuwa dola milioni 600, hii ikiwa ni kiwango kidogo sana cha pesa ikilinganishwa na kipato cha tovuti ya Google.

Hivi karibuni Bw Zuckerberg, alitabiri kuwa idadi ya wanaotumia tovuti yake itafikia billioni moja, lengo ambalo linaweza kufikiwa kwa kuwa katika miezi michache tuu iliopita, watu milioni 100 wapya, walijisajili kwenye tovuti hiyo.

Wadadisi wanasema tovuti hiyo inafanya vizuri licha ya kuwa kuna ishara umaarufu wake umeanza kupungua miongoni mwa watu wa makamo nchini Marekani, ambako ndio ilikuwa ngome ya tovuti hiyo ya Face book.

Kwa sasa tovuti hiyo ni njia muhimu ya mawasiliano kwenye nchi nyingi, ila muasisisi wa tovuti hiyo anasema ongezeko la watumizi halijashuhudiwa nchini Japan, Uchina, Urusi au Korea.

Facebook hata hivyo inakabiliwa na ushindani mkali nchini Brazil na India. Na Licha ya umaarufu huu, tovuti hii imekosolewa sana hasaa kuhusu utaratibu wa kuhifadhi takwimu na taarifa za siri.

Kukosolewa huku kumesababisha watizame upya mikakati yake na kuhakikisha kuna usalama wa kutosha kwenye kurasa zake. Pamoja na hilio Bw Zuckerberg amelazimika kujitetea mahakamani baada ya watu kadhaa kuwasilisha kesi dhidi yake wakidai kuwa wazo la kuanzisha tovuti ya Face book lilikuwa lao.