Polisi: Wanasiasa waepuke fujo TZ

Image caption Tanzania

Jeshi la polisi nchini Tanzania limekutana na vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi mkuu nchini humo mwezi Octoba. Mkutano huo ulilenga kujenga mazingira ya kuaminiana kuliko ilivyokuwa kwenye uchaguzi uliopita.

Polisi wamevitaka vyama kuhakikisha kuwa wafuasi wao wanaepuka vitendo vinavyotishia kulitumbukiza taifa hilo kwenye vurugu.

Vyama vya upinzani vimeelezea kutokuwa na imani na jeshi hilo kwa madai kuwa linaegemea upande wa chama tawala CCM.

Msajili wa vyama vya siasa Tanzania John Tendwa amewaonya wanasiasa kuwa hakuna mgombea atakayevumiliwa kwa kutumia lugha za kibabe,kejeli au matusi kwa kuwa ni kinyume na kanuni za uchaguzi.

"Mtindo wa kuteremsha bendera iliyowekwa kwa namna yoyote ile, au kuharibu kitiu cochote kinachotumiwa kama nembo ya kutambua chama katika kampeini, au kuvisha mbwa fulana za vyama ni kosa," asema bwana Tendwa. Pia ameonya kuwa kosa hilo lina hukumu ya mwaka mmoja gerezani au kutozwa faini ya TSH1,000,000.

Msajili huyo amevitaka vyama vyote 18 vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba kuheshimu makubaliano yatakayoafikiwa kumuunga mkono mgombea yeyote, kwenye urais, ubunge au udiwani.

Naye mkuu wa jeshi la Tanzania Siad Mwema amewataka viongozi wa kisiasa nchini humo kusaidia kutoa elimu ya uchaguzi kwa wananchi ili kudumisha amani iliyopo.