Mapigano yasababisha vifo vya watu 24

Image caption Waasi wa Houthi

Serikali ya Yemen inakabiliwa na ghasia mpya zilizojitokeza kupitia medani mbili.

Takriban watu kumi na tisa waliuawa katika maeneo ya kaskazini ambako waasi wa kabila la Houthi wanahusika.

Wakati huohuo askari watano wa serikali waliuawa katika mapambano na waasi katika shambulio la wapiganaji wenye uhusiano na kundi la Al Qaeda.

Ghasia zilizozuka kaskazini mwa Yemen zinatishia usitishaji mapigano ulioafikiwa mwezi Februari.

Waasi wa kabila la Houthi walipambana na makabila yanayoungwa mkono na serikali wakitumia makombora ikisababisha vikosi vya serikali kuingilia kati.

Ghasia hizi zinafuatia majuma kadhaa ya fujo zilizopooza katika eneo hilo zikisababisha vifo vya watu wengi.

Siku ya Jumanne , kiongozi wa kikabila anayeunga mkono serikali, mtoto wake na mlinzi waliuawa.

Serikali ikalituhumu kundi la Houthi kwa shambulio hilo lakini viongozi wa Houthi wamedai kuwa vifo hivyo vilitokea wakati wa mapigano ambapo nao walipoteza watu kadhaa.

Wahouthi ni wa madhehebu ya Kishia wanaopamabana na serikali ya Yemen yenye ushawishi mkubwa wa Kisunni.

Kuna dhana kuwa Iran inawaunga mkono, ingawa Iran na baadhi ya wadadisi wenye misimamo huru hawakubaliani na dhana hii.

Kusini mwa Yemen, serikali inakumbwa na tatizo tofauti. Huko inapambana na uasi unaodhaniwa kuwa unaungwa mkono na kundi la Al Qaeda.

Katika mashambulio ya hivi karibuni waasi walishambulia na kuua askari watano wa serikali.

Kuna hofu kuwa Yemen inaweza kudumbukia katika mgogoro mkubwa na kugeuka kituo kipya cha kutumiwa na wanaharakati wenye misimamo mikali kwa kuyashambulia mataifa ya magharibi.

Inakisiwa kuwa kiongozi mmoja mwenye msimamo kama huo alishiriki jaribio la kuilipua ndege ya abiria ikiwa njiani kwenda mji wa Marekani wa Detroit siku kuu ya Christmas.