Majeshi zaidi kupelekwa Somalia

Suala la Somalia limetawala vikao vya viongozi wa AU, Kampala
Image caption Suala la Somalia limetawala vikao vya viongozi wa AU, Kampala

Mkutano wa Umoja wa Afrika, AU umeingia katika siku ya pili, kwa viongozi kutoka nchi wanachama wakijadili iwapo nchi zao zipeleke majeshi yao kulinda amani nchini Somalia.

Jumapili, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, aliwataka viongozi hao wa Afrika kushirikiana katika kuwatokomeza wapiganaji wa Kiislam nchini Somalia. Jeshi la kulinda amani nchini Somalia linahitaji askari elfu mbili zaidi.

Mwandishi wa BBC, Afrika Mashariki amesema hapo awali nchi nyingi za Afrika ziliahidi kupeleka vikosi vyao nchini Somalia, lakini hazikufanya hivyo kwa hofu kwamba zingeingia kwenye mgogoro mkubwa wa Somalia.

Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Abukar Abdi Osman, amesema ana uhakika nchi za Afrika zitatuma vikosi zaidi Somalia ili kuliongezea nguvu jeshi la AU nchini humo, AMISOM.

Katika mahojiano na BBC, Bwana Abdi amesema pia anaunga mkono jeshi la AMISOM lipewe madaraka zaidi kwa kuchukua hatua kali dhidi ya wapiganaji wa kiislam wa Al-Shabaab.