Mpinzani mwingine mahakamani Rwanda

Mshtakiwa huyo anadaiwa kupinga mauaji ya kimbari ya mwaka 1994
Image caption Mafuvu ya waathiriwa wa mauaji ya kimbari

Mahakama kuu nchini Rwanda imeanza kusikiliza kesi dhidi ya mwanasiasa wa upinzani Deo Mushahidi.

Mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani kwa madai ya kushirikiana na makundi ya kigaidi, kupinga mauaji ya kimbari na kuhatarisha usalama wa taifa.

Upande wa mashtaka umewasilisha nyaraka kadhaa mahakamani ilikuthibitisha kesi yao dhidi ya Mushahidi. Polisi wanadai Mushahidi aliandika nyaraka hizo ambazo sasa ni kiini kikubwa cha mashtaka saba yanayomkabili .

Lakini mwanasiasa huyo amekanusha mashtaka yote huku akisema ni kesi ya kisiasa. Hata hivyo amekiri kosa la kugushi vyeti vya usafiri, akisema kuwa ilikuwa ni kwa sababu ya usalama wake.

Kuhusu kushirikiana na kundi la FDLR linalotuhumiwa kuwa la kigaidi, Mushahidi amekubali kufanya mashauriano na kundi hilo katika juhudi za kuwezesha maridhiano kati ya kundi hilo na serikali ya Rwanda. Kiongozi huyo wa upinzani amekanusha kushirikiana nalo kwa njia yoyote nyengine kama vile kuanzisha vita nchini humo.

Deo Mushahidi alikuwa mwenyekiti wa shirika la waandishi wa habari nchini Rwanda baaada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na kutoroka nchi hiyo mwaka 2000 hadi Ubelgiji ambako alianzisha chama cha upinzani cha Peoples Democratic Party.

Alikamatwa nchini Burundi mapema mwezi wa tatu na kuhusishwa na mashambulio ya magruneti yaliotokea mjini Kigali wakati huo.

Mahakama imesema kesi yake itaendelea kusikilizwa tarehe 23 Agosti.