Mashindano ya riadha Afrika yaanza Kenya

Makala ya 17 ya mashindano ya riadha barani afrika yanaanza katika uwanja wa Nyayo mjini Nairobi.

Zaidi ya wanariadha 700 wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo ya siku tano.

Image caption Mrusha kisahani wa Algeria akipasha moto viungo ndani ya uwanja wa Nyayo mjini Nairobi.

Kuangalia picha zaidi bofya hapa.

Kutakuwa na raundi ya kwanza ya mbio kadhaa, huku medali za kwanza za mashindano hayo zikitolewa kwenye wa fainali za mbio za mita 400 kuruka viunzi, fainali ya kurusha tufe na mbio za mita 10,000 kwa wanaume.

Mapambano makali

Mbio za mita 10,000 kwa wanaume zinatarajiwa kuwa na upinzani mkali.

Kenya itawakilishwa na Wilson Kiprop, Geoffrey Mutai na Mathew Kisorio. Uganda itakosa huduma za mwanariadha wake Boniface Kiprop lakini bendera ya Uganda itapeperushwa na Geoffrey Kusuro, Abraham Kiplimo na Moses Kipsiro.

Mahasimu wa jadi wa Kenya, Ethiopia nayo itawakilishwa kwenye mbio hizo na Sileshi Sihine na Tariku Bekele.

Mbio nyingine ambazo zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali ni pamoja na mbio za raundi ya kwanza za mitan 100, mita 400 na mita 800 kwa upande wa wanaume na kina dada.

Mbio fupi

Katika mbio za masafa mafupi, wanariadha kutoka Nigeria wanatarajiwa kuwika huku Obinna Metu, Ogbo Ogen Egweru na Benjamin Adukwu wakitarajiwa kufanya vyema katika mbio za mita 100.

Wanariadha hao watakuwa wakijaribu kuvunja rekodi ya mashindano hayo ya sekunde tisa nukta tisa nane inayoshikiliwa na mnaigeria Olusoji Fasuba.

Rais Mwai Kibaki anafungua rasmi mashindano hayo.

Kuangalia picha bofya hapa

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii