Hali ya usalama Darfur yazidi kuzorota

Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inasema kwamba machafuko yaliongezeka huko Darfur mara tu baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa kitaifa mwezi wa Aprili mwaka huu huko Sudan.

Katibu Mkuu huyo Ban Ki Moon amesema, katika mwezi wa Mei pekee, zaidi ya watu 400 waliuawa katika mapigano kati ya vikundi vya waasi na majeshi huko Darfur.

Image caption Makundi ya waasi yameshutumiwa kuendeleza mapigano huko Darfur

Ghasia hizo zimeripotiwa licha ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika kupeleka majeshi ya kulinda amani katika eneo hilo miaka mitatu iliyopita.

Ban Ki Moon anahofia kwamba kujiondoa katika meza ya mazungumzo kwa kundi la JEM kunaweza kutatiza kupatikana kwa suluhisho la mzozo wa jimbo hilo.

Anaeleza kwamba bila ya kuwepo kwa muafaka wa amani wa Darfur, kuna wasiwasi wa Sudan kuendelea kukumbwa na hali ya ukosefu wa usalama, hasa wakati huu ambapo nchi hiyo inakaribia kushiriki kura ya maoni kuhusu hatma ya Sudan Kusini kujitenga au kuendelea kuwa sehemu ya Sudan.

Machafuko huko Darfur yalianza mwaka 2003 baada ya waasi wenye asili ya Kiafrika kuanza kupambana na majeshi ya Serikali kwa madai kwamba eneo lao limepuuzwa.