Bennet: Zimbabwe inatawaliwa kijeshi

Mmoja wa wabunge wa bunge la Zimbabwe, Roy Bennett, ambaye ni mzungu ameiambia BBC kuwa anaamini kwa sasa Zimbabwe inaendeshwa na utawala wa kijeshi.

Bwana Bennett, ambaye ni mshirika wa karibu wa waziri mkuu, Morgan Tsvangirai, amesema anaamini Rais Mugabe analazimishwa na jeshi kuendelea kutawala nchi hiyo.

Image caption Rais Mugabe amedaiwa kuliachia jeshi uongozi

Bwana Bennett, ambaye ni mkulima wa zamani, amezuiliwa kuchukua wadhifa wa unaibu waziri wa kilimo katika serikali ya umoja wa kitaifa kutokana na taratibu za kisheria zinazorudiwa rudiwa.

Matamshi hayo yametolewa wakati ambapo mpango wa kukusanya maoni kuhusu katiba mpya nchini Zimbabwe umegubikwa na taarifa za ghasia katika eneo la jimbo la magharibi la Mashonaland.

Kuna madai kwamba watu wanalazimishwa kuhudhuria mikutano ya usiku, na watu maalum huteuliwa kutoa maoni ambayo hufanana na msimamo wa chama cha ZANU PF cha Rais Robert Mugabe.

Wafuasi wa chama cha Movement for Democratic Change or MDC wanasemekana kuzuiwa kuhudhuria mikutano hiyo ya kutoa maoni. Wengine wameripotiwa kulazimishwa kuhama jimbo hilo.