Wapiganaji wa Kisomali wasitisha maasi Ethiopia

Bendera ya Ethiopia
Image caption Bendera ya Ethiopia

Serikali ya Ethiopia leo inatarajiwa kusaini mkataba wa maridhiano kati yake na kundi la waasi la United Western Somali Liberation Front.

Kundi la UWSLF mwezi April mwaka huu lilikubali kuweka chini silaha zao baada ya mazungumzo ya siri kati yake na serikali ya mjini Addis Ababa. Kukubali kwa muafaka na serikali, kundi hilo linamaliza miongo miwili ya harakati za kijeshi dhidi ya serikali , wakati huo likiwa na nia ya kujitenga na Ethiopia.

Asili ya kundi hilo inahusishwa na kundi la Western Somali Liberation Front, ambalo wakati huo liliungana na majeshi ya Somalia dhidi ya Ethiopia katika vita vya Ogaden mwaka wa 1977.

Wakati huo wanachama wengi wa kundi hilo walikuwa Somalia, na hata baadhi yao kupatiwa nyadhifa mbali mbali serikalini kama mawaziri na hata maafisa waandamizi jeshini.

Serikali ya Ethiopia inayoongozwa na chama cha EPRDF cha Waziri Mkuu, Meles Zenawi, imekuwa ikipigana na makundi ya Kisomali katika jimbo la Ogaden, likiwemo kundi hili la UWSLF.

Kutia saini mkataba na kundi hili, kunamaanisha kuwa Ethiopia inajipunguzia mzigo wa mapambano na makundi ya waasi na kuweza kusaidia ujenzi na maendeleo katika jimbo la Ogaden lenye maendeleo duni nchini Ethiopia.

Wiki kadhaa zilizopita serikali ya Ethiopia iliweza kufanya mazungumzo na kundi la ONLF lililogawanyika, ambalo nalo linapigana na serikali kwa lengo la kukomboa mkoa wa Ogaden.

Lakini, kiongozi wa kundi hilo Gen Mohamed Omar Osman, amesema wajumbe waliofanya mazungumzo na serikali ya Ethiopia hawana ridhaa ya kundi hilo, na akaongeza kuwa baadhi ni wafungwa waliolazimishwa kuzungumza na vyombo vya habari.

Ikiwa serikali ya Ethiopia ina nia njema ya kumaliza vita katika jimbo la Ogaden huenda hatimaye makundi yaliyobaki ya waasi yakasalimu amri au kufikia muafaka na serikali, lakini hofu iliyopo ni kuwa uwezekano wa kuzuka kwa mapigano kati ya makundi ya waasi, haswa yale yaliyotia saini mkataba na serikali na yale yanayopinga.