Shughuli ya uokoaji yaendelea Congo

Wafanyakazi wa uokoaji wanawatafuta manusura wa ajali ya boti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo watu themanini walikufa baada ya boti hiyo iliyobeba abiria kuzidi uwezo wake na kuzama mtoni.

Image caption Ramani ya Kongo kuonyesha maeneo husika na ajali ya boti.

Boti hiyo iliyokuwa na wafanyakazi na abiria wapatao 200 inaaminika kugonga kingo za mchanga au mwamba siku ya Jumatano katika maunganiko ya mto Congo, kwenye jimbo la Bandundu lililopo magharibi mwa nchi hiyo.

Baada ya miongo kadhaa ya migogoro, Kongo ina barabara chache au huduma za reli, hali inayosababisha wengi kusafiri kwenye boti hizo zilizojaa pomoni.

Mara kwa mara

Mwezi Novemba mwaka jana, takriban watu 73 walifariki dunia baada ya boti kuzama kwenye ziwa, pia katika jimbo la Bandundu.

Ajali iliyotokea hivi karibuni ilitokea siku ya Jumatano.

Boti hiyo ilikuwa ikibeba abiria na bidhaa kutoka Mushie, takriban kilomita 30 kutoka Bandundu, mji mkuu katika jimbo hilo.

Ofisa polisi wa jimbo hilo Jolly Limengo, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba: " Boti hiyo ilijaa pomoni na haikuweza kuhimili kupita kwenye dhoruba hiyo."