Moi aambiwa amheshimu Kibaki

Rais wa zamani wa Kenya Daniel Arap Moi ameambiwa na kamati ya kujenga usalama, kuwa amheshimu rais aliyeko madarakani, kufuatia wawili hao kushambuliana kwa maneno katika moja ya kampeni kuhusu katiba.

Image caption Daniel Arap Moi, Rais wa zamani wa Kenya

Rais Mwai Kibaki anataka wananchi wa Kenya kuupitisha muswada wa katiba mpya, huku Bw. Moi akiongoza kampeni ya kupinga katika hiyo.

Lakini kamati iliyoundwa ya kujenga utaifa imesema mzozo huo wa kibinafsi unaathiri kazi zake.

Baadhi wanahisi Kenya huenda ikarejea katika hali iliyotokea mwaka 2007 na 2008 baada ya kufanyika uchaguzi ambapo watu zaidi ya elfu moja waliuawa na wengine laki 3 kukosa makazi.

Image caption Rais Mwai Kibaki

Siku ya Alhamisi, Bw. Moi ambaye aliwahi kuwa rais wa Kenya kwa miaka 24 alisema Bw. Kibaki hatakiwi kumshutumu kwa kupinga muswada huo, kwa kuwa hakutimiza ahadi yake ya kubadili katika ndani ya siku 100, wakati alipoingia madarakani mwaka 2002.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya kujenga utaifa (NCIC) Mzalendo Kibunjia amemtaka Bw. Moi kumheshimu rais na kutoa wito kwa Bw. Moi na Bw. Kibaki kujizuia kutoa matamshi ambayo yanaweza kusababisha mvutano katika kampeni za kura hiyo ya maoni.

Image caption Ghasia za mwaka 2007-8

Kura ya maoni itafanyika Agosti 4.

Watu wasiopungua sita waliuawa baada ya bomu la kurushwa kwa mkono kutupwa katika mkutano wa kampeni ya kupinga rasimu hiyo mwezi Juni mjini Nairobi, huku wabunge watano wakishitakiwa kwa kutoa matamshi ya chuki wakati wa kampeni hizo. Hatua hiyo ilifuatua malalamiko yaliyofikishwa kwa NCIC.

Ghasia nyingi za mwaka 2007-8 zilitokea wakati uhasama katika uchaguzi ulipozusha mizozo ya kugombea ardhi, hasa katika eneo la Bonde la Ufa, sehemu anayotoka Bw. Moi.

Moja ya kipengele katika rasimu ya katiba mpya, ni kuunda tume ya ardhi ambayo itataifisha ardhi iliyopatikana kwa njia zizozo halali wakati wa utawala wa rais Moi.