Kura ya maoni Zanzibar yakaribia kupita

Ramani ya Tanzania kuonyesha Zanzibar.
Image caption Ramani ya Tanzania kuonyesha Zanzibar.

Matokeo ya awali yameanza kutolewa, baada ya kura ya maoni iliyopigwa visiwani Zanzibar, inayolenga kubadili katiba ili kuruhusu vyama hasimu kuunda serikali za muungano, na kumaliza miongo kadhaa ya uhasama mkubwa wa vyama vya kisiasa.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa aslimia 65 ya wapiga kura wanaunga mkono mabadiliko hayo ya katiba, na hivyo kuashiria matumaini ya ukurasa mpya wa kisiasa kufunguliwa Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chama tawala - CCM na kile cha upinzani CUF, vilitoa wito kwa watu kuunga mkono mabadiliko hayo na kupiga kura ya ndiyo, baada ya uhusiano wa vyama hivyo viwili kuonekana kuimarika kwa awamu.

Tume ya uchaguzi imesema upigaji kura umekuwa salama.

Tume hiyo inatarajia kuwa idadi ya watu waliopiga kura inaweza kufika karibu asilimia tisini.

Ghasia na umwagikaji damu zimekuwa zikitawala uchaguzi wa Zanzibar katika siku za nyuma.

Kisiwa cha Zanzibar, kina utawala wake wa ndani chini ya Jamhuri ya Tanzania.

Ikiwa kura hiyo ya maoni itapitishwa rasmi, katiba itafanyiwa marekebisho kwa haraka kwa ajili ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi October mwaka huu.