Erikson akataa kubaki Ivory Coast

Wakuu wa chama cha mpira cha Ivory Coast wanasema wameshindwa kumshawishi kocha aliyeiongoza timu hiyo kwenye Kombe la Dunia huko Afrika ya kusini, Sven Goran Erikson kubaki kama mkufunzi wao.

Hii ni kutokana na kiwango cha mshahara anaodai Bw Erikson.

Image caption Kocha Erikson akiwasimamia wachezaji wake wakati wa Kombe la Dunia.

Msemaji wa chama cha mpira cha Ivory Coast, Sory Diabate amesema ingawa pande zote zimekubaliana kwa masuala yote ya soka wameshindwa kuafikiana juu ya malipo.

Itakumbukwa kuwa Erikson aliajiriwa mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu kuiongoza Ivory Coast katika fainali za mwaka huu huko Afrika ya kusini.

Huku timu hiyo kama nyingi za Afrika, zilitoka na matokeo yasiyo ya kuridhisha na hata kushindwa kupiga hatua ya 16.

Kati ya timu hizo ni Ghana pekee iliyosonga mbele na kuondolewa katika hatua ya 16 na Uruguay.

Diabate amesema chama cha mpira nchini Ivory Coast kwa sasa kinafanya mazungumzo na makocha wengine na wana imani watamtangaza kocha mpya katika siku chache zijazo.

Aliongezea kusema mambo yote yatatulia kabla ya ziara ya jiji la London ifikapo tarehe 7 Agosti kwa mechi ya kirafiki na Italia.

Magazeti ya huko yanasema kuwa chama hicho sasa kinazungumza na kocha wa club ya Ufaransa, Olympique Marseille Gerard Gili kuchukua nafasi hiyo.