Mmoja wa waasisi wa SPLM afariki dunia

Salva Kiir

Watu wa kusini mwa Sudan wanaomboleza kifo cha aliyekuwa waziri Samson Kwaje ambaye alifariki baada ya kupata matatizo ya figo. Kwaje alikuwa mfuasi na msemaji wa kundi la waasi wa SPLM wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka ishirini na miwili.

Kulikuwa na hofu kubwa baada ya kifo cha waziri Samson Kwaje kutangazwa wakati wa ibada ya misa katika kanisa kuu mjini Juba.

Kwaje alikuwa mwanasiasa maarufu kusini mwa Sudan baada ya kuunga mkono kundi la waasi la Sudan People's Liberation Movement (SPLM) kwa zaidi ya miaka ishirini wakati wa vita kati ya Sudan Kaskazini na Kusini.

Kama msemaji wa SPLM, Kwaje alijulikana kimataifa kama sauti ya watu wa Kusini mwa nchi hiyo wakati walipokuwa waking'ang'amia usawa na Sudan Kaskazini.

Aliwahi kuhudumu kama waziri wa serikali na hivi karibuni alikuwa akiongoza kampeni ya kuchaguliwa kwa rais Salva Kiir.

Afisa mmoja wa serikali alisema kuwa Samson kwaje alifariki hapo jana akiwa hospitalini mjini Nairobi lakini hakutoa maelezo zaidi.

Mwezi Novemba mwaka jana alijeruhiwa wakati majambazi waliposhambulia msafara wake kusini mwa Juba lakini aliponea chupuchupu huku wenzake wakiuawa.

Raia wenhi wa Kusini wanasikitika sana kuwa licha ya kuwa mstari wa mbele wa ukombozi, Samson Kwaje hakuishi kuona matokeo ya kura ya maoni itakayoamua ikiwa Sudan Kusini itajitawala au la.