'Mchina kuinunua Liverpool'

Liverpool huenda ikanunuliwa na mfanyabiashara kutoka Uchina, na vyanzo karibu na mnunuzi huyo vinasema, makubaliano yanakaribia kufikiwa.

Image caption Mashabiki wa Liverpool

Kenny Huang, ambaye ni mkuu wa kampuni ya QSL Sports yenye makao yake huko Hong Kong, anataka kuchukua umikili kamili ya Liverpool, ambayo imekuwa ikiuzwa tangu mwezi Aprili.

"Makubaliano hayana budi kufikiwa kabla ya msimu wa usajili kumalizika [Agosti 31}" kimesema chanzo hicho kwa BBC.

"Huang amewasilisha maombi ya ununuzi. Bodi ya klabu hiyo inatakiwa kutathmini mauzo hayo na huenda ikatokea katika siku chache zijazo" kimesema chanzo hicho.

Image caption 'Mnunuzi mwenye nia'- Kenny Huang

Huang amekuwa na mazungumzo kwa wiki kadhaa na wawakilishi wa Benki ya Scotland, RBS, akiwa na lengo la kuchukua umiliki kamili wa klabu hiyo ya ligi kuu ya England.

Deni kubwa la Liverpool liko RBS, linalofikia pauni milioni 237, kutoka kwa wamiliki wa Kimarekani Tom Hicks na George Gillett.

"Kenny ni mnunuzi mwenye nia na klabu hiyo na ana matumaini" kimesema chanzo hicho.

Huang anataka kulipa deni la Liverpool kwa RBS na kumkabishi meneja mpya Rot Hodgson fedha za kununua wachezaji katika msimu huu wa usajili.

Image caption Roy Hodgson 'kupewa fungu'

Tajiri huyo wa Uchina ana mipango ya kujenga uwanja mpya hara iwezekanavyo.

Huang aliripotiwa kukataa kununua klabu ya Liverpool mwaka 2008 kwa sababu alihisi bei ya pauni milioni 650 ilikuwa ya juu mno. BBC idara ya michezo ina taarifa kuwa tajiri huyo anaithamanisha klabu hiyo kwa pauni milioni 350.

Hicks na Gillett waliinunua Liverpool mwezi Februari mwaka 2007 kwa pauni milioni 218.9 huku madeni yakiwa pauni milioni 44.8.