18 wateketea kwa moto Afrika Kusini

Maafisa wa huduma za dharura wamesema moto katika nyumba wanaoishi wastaafu nchini Afrika Kusini umesbabisha vifo vya watu 18.

Image caption Afrika Kusini

Taarifa zinasema wengine kadhaa walijeruhiwa kufuatia moto huo ulioanza saa tatu usiku saa za Afrika Kusini, siku ya Jumapili.

Nyumba hiyo iko kilomita 50 kusini mashariki mwa Johannesburg.

Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.

Vyombo vya habari vya huko vimesema wazee 84 wanaoishi waliokolewa na kupelekwa katika kanisa moja, huku wengine kadhaa wakipatiwa matibabu.

Taarifa za moto huo zilitolewa na walinzi walioona moto ukiwaka ndani ya jengo.

"Jengo lilikuwa limeghubikwa na moto, na maafisa wa huduma za dharura walijitokeza kuwasaidia wazee wanaoishi humo", amesema msemaji wa huduma za dharura Chris Botha.

Baada ya moto kuzimwa wafanyakazi wa huduma za dharura walipata mabaki ya miili 17 ya watu walioungua.

Mtu wa 18 alifariki kwa kile kinachodhaniwa kuwa ni ugonjwa wa moyo, muda mfupi baada ya kuokolewa.

Taarifa zinasema mtu mwingine alipelekwa hospitali mjini Johannesburg kwa kutumia helikopta.

Mlinzi mmoja amewaambia waandishi wa habari jinsi alivyojitahidi kuokoa wazee wanaoishi katika jengo hilo.

"Labda niliokoa wanane au tisa, lakini wengine walikuwa wazito na sikuweza kuwabeba" amesema mlinzi huyo akizungumza na shirika la habari la Urafansa.