Vigogo waanguka uchaguzi wabunge CCM

Matokeo yasiyo rasmi kutoka Tanzania, yanaonyesha kuwa baadhi ya wanasiasa wakongwe au vigogo wa chama tawala cha CCM wamepigwa kumbo katika kura za maoni kuchagua wabunge ndani ya chama hicho.

Toa maoni yako

Mchakato huo mkali uliofanyika siku ya Jumapili umesababisha kuanguka kwa John Malecela, aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania, akigombea jimbo la Mtera ameangushwa na Livingstone Lusinde. Kinachofurahisha zaidi ni kwamba Malecela na Lusinde ni ndugu.

Wabunge sita nje mkoa mmoja

Mkoa wa Iringa umeshuhudia wabunge sita wakishindwa kutetea viti vyao, katika jimbo la Njombe Kaskazini, Jackson Makweta ambaye amekuwa mbunge tangu mwaka 1970, ameangushwa na mfanyabiashara Deo Sanga. Bw Makweta aliwahi kuwa waziri miaka ya nyuma.

Kigogo mwingine aliyepokonywa heshima ya ubunge Joseph Mungai - jimbo la Mufindi Kaskazini, aliyewahi kuwa waziri wakati serikali ya rais wa kwanza, Julius Nyerere.

Wengi walioangushwa ni Profesa Raphael Mwalyosi (Ludewa), Benito Malangalila (Mufindi Kusini), Yono Kevela (Njombe Magharibi) na Monica Mbega (Iringa Mjini).

Anna Tibaijuka aliyekuwa msaidizi wa katibu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na makazi, alimpiga mweleka Wilson masilingi.

Mawaziri

Aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Diodorus Kamala ametupwa katika kura za maoni kuwania jimbo la Nkenge.

Baadhi ya Mwaziri waliokabiliwa na upinzani lakini wamepita ni Profesa David Mwakyusa (Afya) na John Chiligati (Ardhi).

Sura za vijana

Miongoni mwa sura mpya ni kijana January Makamba aliyemwangusha William Shelukindo, mbunge anayemaliza muda wake jimbo la Bumbuli na kigogo wa CCCM.

Vile vile yupo mtangazaji wa VOA ya Marekani, Juma Nkamia ameshinda maoni jimbo la Kondoa Kusini baada ya kumwangusha mwanasiasa mkongwe Pascal Degera.

Mwingine ni mwandishi wa habari, Deo Filikunjombe, aliyemtosa Profesa Mwalyosi wa jimbo la Ludewa.

Matokeo rasmi yatapatikana hivi karibuni, ingawa hata walioshinda hawana uhakika asilimia 100 wa kuwakilisha Chama Cha Mapindunzi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Wote watalazimika kusubiri kikao cha Kamati Kuu ambacho kina mamlaka na idhini ya kufuta wagombea watakaobainika kuwa wamekiuka taratibu za chama hicho - ikiwa ni pamoja na kutoa rushwa kwa wapiga kura, jambo ambalo limedaiwa kujitokeza mara nyingi katika mchakato wa kura za maoni.

Kamati Kuu itakutana tarehe 14 Agosti.

Maoni Yenu

Uchaguzi umepita lakini inasikitisha kuona wananchi wamebadilika dakika za mwisho kwa kupewa simu za mikononi na fedha kidogo za vocha. Lakini wananchi walio wengi waliuligundua na wachache hawakuligundua baada ya TAKUKURU kulala usingizi kwa kukosa ushahidi wakiwa ofisini wakati Rusha toka kwa wagombea ilikuwa nje nje, katika majimbo mengi ya Tanzania. Alphaxard - Tabora, Tanzania.

Nimefurahi kuona matokeo ya mkoa wa Iringa, maana wananchi wameamua kufanya mabadiliko kamili, tukianzia na Mufindi, Kalenga na Iringa Mjini. Mwakalindile - Mbeya, Tanzania.

Matokeo ni imani ya wananchi kwa wagombea wao, hongereni wakazi wa Kalenga na majimbo yote ya Iringa kwa uamuzi wa busara. Kalinga - Iringa, Tanzania.

Hongera kwa wananchi wote wa Tanzania waliozitendea haki kura zao za maoni kwa kuwachagua watu wenye imani nao.Kama uongozi wa CCM utawarudisha au kuwapitisha watu wa chaguo lao na si la wananchi,

nina imani kubwa wananchi watafanya maamuzi ya busara zaidi ya haya kwenye uchaguzi mkuu wa October.Zaidi,HONGERENI sana BBC kwa mfumo mzuri wa upashaji habari kupitia ukurasa huu... Mlimira Z.R - Dar Es Salaam, Tanzania.

Ukweli demokrasia katika chama cha mapinduzi imekua kwa kiasi kikubwa sana kwani ni mda mrefu sasa baadhi ya wanasiasa wakongwe ambao walianza kufanya mambo kwa uzoefu badala ya kushughulisha

vichwa vyao kubuni mambo yatakayosaidia kuleta maendeleo ya nchi.Tunashukuru mheshimiwa rais ameleta mwarobaini wao.kiongozi akilewesha tunatupa kuleeeee! Kelvin Msawile - Morogoro, Tanzania.

Nina furaha sana kuishuhudia nchi yangu ikibadilika katika historia ya siasa. Kweli waTanazania kumbe twaweza sisi wenyewe bila ya vitisho na kumbe historia pia inahesabika kwani wagombea kushinda

kulikuwepo na ubadhirifu wa aina nyingi ikiwepo kuiba kura na kutoa rushwa.Hongera wananchi wa Tanzania, kwa pamoja tunaweza tukiamua. Richard - Dubbo, Australia.

Wabunge wote wa zamani wazee bado wanatukatalia kurundi nyumbani kwa kutoruhus kuwa na uraia wa nchi mbili.Kama nchi zote za jumuia ya madola. Noah - London, UK

Naomba viongozi wa Africa ikiwemo Tanzania waache uroho wa madaraka maana wengine wameshakaa madarakani zaidi ya miaka ishirini wawaachie wengine na kushindwa kwao isiwe tabu kwetu maana hiyo ndio demokrasia ya uchaguzi na asiye kubali kushindwa sio mshindani,achia mwenye madaraka ili upate kuheshimiwa na jamii sio kuwa king'ang'anizi wa madaraka. Emmanuel Dawson Moshi - Dar Es Salaam, Tanzania.

Demokrasia ya kweli iko wapi AfriKa ya Mashariki? Hususan wakati huu wa chaguzi? Rushwa na vitimbi kila kona, na hata modality ya kuwachagua wagombea wa nafasi tofauti katika serikali si ya kidemokrasia. Kwa nini wananchi wasiwachague viongozi moja kwa moja? Badala ya kura za maoni? Tunatakiwa tubadilike kama wenzetu wa Ulaya na marekani ili demokrasia ya kweli itendeke.

Kuna mianya mingi sana ya rushwa na takrima katika mchakato wa kuwatafuta wagombea wa nafasi katika chaguzi zetu. Aristarik Hubert Maro - Kampala, Uganda.

Tunafurahia sana BBC inavyokuwa ya kwanza hata kabla ya vyombo vya habari vya hapa kutupasha habari hasa kuhusu mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu 2010 Tanzania. Endeleeni hivyo hivyo. Exaud John Makyao - Moshi, Tanzania.

Watanzania tunaihitaji mabadiliko kiti cha ubunge sio cha mtu mmoja, kazi ikikushinda kaa pembeni kwa heshima na uwaachie wengine wapokee kijiti cha kuendesha maendeleo ya nchi.Tabia ya kung'ang'ania madaraka sio nzuri.Hongera sana CCM kwa mchakato mzuri lakini mjihidi kuheshimu maamuzi ya wanachama mliowapa lidhaha ya kuchagua. Emmanuel Salila – Dodoma, Tanzania.

Kuanguka kwa vigogo wa CCM ni dalili njema kwa nchi yetu kwani wananchi wameanza kuelewa kuwa mabadiliko ya kisiasa ni muhimu ili kujiletea maendelea na CCM wakijidanganya kuwarudisha waliokataliwa na wananchi watajutia uamuzi wao.Huku kwetu Rukwa nako wameangushwa wabunge wanaomaliza muda wao kama ludovick mwananzilla (Kalambo), Nyami (Nkasi) na Elieta Switi (Sumbawanga Mjini).

Ladislaus David - Sumbawanga, Tanzania

Napenda kutoa maoni na kupendekeza kuwa ni bora viongozi kama hao ambao hawapendi maendeleo ya wananchi waache kuongoza majimbo, hakuna mabadiliko katika majimbo yao kwanini tokea miaka ya 1970 mpaka leo 2010 hali ni ile ile enzi za mwalimu (ufisadi umekithiri).

Athuman Hamido Nyinji - Lichinga, Msumbiji

Hii ngumi mkononi kura za maoni CCM inamaanisha nini mbele ya watanzania? James Massawe - Tanga, Tanzania

Nampongeza mwana harakati Juma Nkamia kwa kushinda katika kura za maoni huko Kondoa, pia nampongeza mhe John Magufuli kwa kuwabwaga wapinzani wake huko chato, pia nampongeza mpiganaji kijana Lawrence Masha kwa kuibuka kidedea hapa wilaya ya Nyamagana.Pia BBC mko juu kwani mnanifurahisha jinsi mnavyo tuwekea habari katika kurasa hizi.......

Boniphace Maiga Juma - Butimba TTC – Mwanza, Tanzania

Naiomba NEC kuwafuta wagombea wote ambao watabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa. Kama mgombea ana uwezo kwanini atoe rushwa?CHEMA CHAJIUZA NA KIBAYA CHAJITEMBEZA. Wananchi msikubali kununuliwa kwa vijisenti na kuteseka kwa miaka 5. Mary Mamsindo - Dar Es Salaam, Tanzania

Pongezi kwa BBC kwa kutoa habari motomoto.Pongezi pia kwa mtangazaji maarufu nchini Tanzania (Juma Suleman Nkamia) kwa kupata tiketi kura za maoni - Kondoa Kusini. BBC endelea kutupa habari zaidi.

Ludovick Swai – Dodoma, Tanzania

Mimi hata kama siyo Mtanzania naomba nichangie mawazo yangu pamoja na ndugu zangu wa Tanzania.Kumbukeni kwamba CCM imetawala miaka nyingi sana yakiwa madarani bila hata mabadiliko ya nchi.Nikiangalia nchi za Afrika ya Kati na mashariki hali ni moja tu.Kwani wale wote walio wai kutumika zamami ndio wenyewe wanazoe kula rusha mara kwa mara.Lakini kukiwa na mabadiliko naamini rushwa itapunga ujambazi vile vile tabia mbaya ya jeshi la polise ubakaji mauwaji yakiolela yote yamo katika ulaji rushwa.

Selemani Bishibe – Gothenburg, Sweden

Ni ukomavu wa kisiasa kwa wananchi kuchagua watu wale wanaowataka kwani wao ndio wanaowafahamu. Serikali isilazimishe kuwarudisha wale wote walioshindwa kwani maamuzi ya wana CCM ya wale waliowachagua.

Revo Madeni - Dar Es Salaam, Tanzania

Tanzania demokrasia imekua, twaishuhudia Tanzania mpya! Kwanza niwapongeze wazanzibari kwa kupiga kura ya ndiyo kuunda serikali ya mseto. Pili tumeshuhudia wananchi wakituletea sura mpya katika chaguzi mbalimbali kupitia kura za maoni katika vyama tofauti, hakika ni jambo la kujivunia. Ila dosari zilizojitokeza katika hizi chaguzi hazina budi kushughulikiwa ipasavyo katika ngazi husika, ikiwa ni pamoja na masuala ya rushwa katika chaguzi.

Lameck Kakulu - Tokyo, Japan

Toa maoni yako

Mitandao inayohusiana

BBC haina haihusiki vyovyote na taarifa za mitandao ya kujitegemea