Amani yahimizwa wakati wa kura ya maoni Kenya

Wananchi wa Kenya wanapiga kura muhimu ya maoni kuamua hatma ya katiba mpya ya taifa hilo la Afrika Mashariki, huku viongozi wakitoa wito wa amani kote nchini humo.

Picha za kura ya maoni

Kura hii ya maoni inafanyika miaka miwili baada ya mamia ya watu kuuawa katika ghasia zilizozuka punde baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Katiba mpya imelenga kubadilisha mfumo wa siasa za Kenya na kuzuia kutokea tena kwa ghasia hizo zilizosababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao. Kura ya maoni imeonyesha kuwa katiba hiyo itakubaliwa na wananchi. Wanaoiunga mkono katiba wanasema kuwa itachangia ugawanaji wa mamlaka kwa kuunda utawala wa majimbo, kumaliza ukabila na pia kusuluhisha au kuleta mabadiliko katika sera ya ardhi.

Miongoni mwa viongozi waliotoa wito wa amani wakati wa shughuli hiyo ni rais Mwai Kibaki, Waziri mkuu Raila Odinga na viongozi wa tume ya muda wa uchaguzi nchini humo, IIEC.

Picha za kura ya maoni