Marufuku kumpiga picha Naomi - Hague

Naomi Campbell
Image caption Naomi Campbell

Majaji huko the Hague wamekataza mwanamitindo maarufu Naomi Campbell kupigwa picha anapotoa ushahidi katika kesi ya aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor.

Bi Campbell, mwenye umri wa miaka 40, anatarajiwa kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo ya uhalifu wa kivita siku ya Alhamis.

Mwendesha mashtaka itamwuuliza juu ya madai kuwa Bw Taylor alimpa 'almasi haramu zinazotumika kugharamia vita' ambazo hazijachongwa kutoka Sierra Leone baada ya shughuli ya chakula cha jioni cha watu maarufu iliyofanyika mwaka 1997.

Pia ataruhusiwa kupata msaada wa ziada kutoka kwa wakili wake wakati anapotoa ushahidi wake.

Mawakili wake wataruhusiwa kuingilia kati ili kumzuia asije kujibu swali ambalo litasababisha ajitie matatani mwenyewe.

'Wasiwasi'

Wapiga picha watazuiwa kupiga picha wakati anapoingia na kutoka ndani ya mahakama hiyo.

Imeripotiwa kuwa, kesi hiyo itaonyeshwa kupitia televisheni jinsi inavyoendelea kama ilivyo desturi.

Image caption Charles Taylor

Hatua za kuwalinda mashahidi aghlabu hutolewa katika kesi za uhalifu wa kivita iwapo kuna ishara za mashahidi kuwepo hatarini, au familia zao baada ya kutolewa ushahidi huo.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo ilisema shauku kubwa ya vyombo vya habari katika kesi hiyo imesababisha kuwepo "kwa sababu za kuwepo wasiwasi" wa usalama wa Bi Campbell.

Bw Taylor anatuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika kipindi cha miaka 10 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sierra Leone.

Upande wa mashtaka umesema Bw Taylor aliwapa silaha kundi la waasi la Revolutionary United Front (RUF) na badala yake akawa anapewa almasi kutoka kwenye migodi iliyokuwa ikidhibitiwa na waasi.

Amekana mashtaka na alisema hajawahi kuhusika na lolote kuhusiana na almasi.

Lakini upande wa mashtaka ulisema wakati vita vikiendelea Sierra Leone, Bi Campbell na Bw Taylor wote walikuwa wageni waalikwa katika shughuli iliyoandaliwa na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela.

Baada ya chakula hicho cha jioni, inadaiwa kwamba, wafuasi wawili wa Bw Taylor walikwenda kwenye chumba cha Bi Campbell na kumpa almasi kubwa ambayo haikukatwa.