Wapinzani wakubali kushindwa Kenya

Waziri Willium Ruto
Image caption Waziri Willium Ruto

Viongozi walioongoza kampeni za kupinga katiba mpya inayopendekezwa nchini Kenya, wamekubali kuwa wameshindwa katika kura ya maoni.

Huku idadi kubwa ya kura ikiwa imehesabiwa, matokeo ya mapema yanaonyesha kuwa takriban 70% ya wapigaji kura wameunga mkono katiba hiyo inayolenga kupunguza mamlaka ya rais.

''Wengi wameonyesha msimamo wao, na sisi pia tumeonyesha msimamo wetu, sasa tunatoa witu kuwepo mashauriano,'' amesema waziri wa elimu ya juu Willium Ruto wakati akikubali ushindi wa upande uliounga mkono katiba hiyo.

Katiba hiyo mpya inayopendekezwa, inaonekana kupingwa vikali katika mkoa wa Rift Valley ambao uliathiriwa pakubwa na machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Katiba hiyo, imeundwa ili kuzuia hali machafuko kama hayo kutokea tena, na pia kushugulikia maswala muhimu kama ya ardhi.

Waziri Ruto, ambaye ana nuia kugombea Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2012, amekuwa akipinga vipengele vinavyohusu uavyaji mimba na pia ardhi.

Rais Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga, waliongoza kampeni ya kuunga mkono katiba hiyo.

Shugli nzima ya kupiga kura hiyo ya maoni hapo jana ilifanyika kwa njia ya amani na hakuna matukio makubwa yaliyoripotiwa katika jumla ya vituo 27,000.

Gazeti la The Standard, la nchini Kenya limesema kuwa shugli hiyo imeonyesha ''mwamko mpya'' kwa Kenya.

Nalo gazeti la Daily Nation, limewataka watu waliopinga katiba hiyo kukubali kushindwa.

Kenya sasa inakabiliwa na kibarua kigumu cha kutekeleza mabadiliko yaliyojumuishwa katika katiba hiyo mpya.