Rais wa zamani wa Uganda afariki dunia

Image caption Godfrey Binaisa

Aliyekuwa Rais wa Uganda Godfrey Lukongwa Binaisa amefariki dunia.

Amefariki dunia asubuhi nyumbani kwake mjini Kampala akiwa na umri wa miaka 90.

Mwanafamilia mmoja alisema alikufa usiku wa manane nyumbani kwake katika viunga vya mji huo.

Binaisa aliyezaliwa Mei 30, 1920, alikuwa mwanasheria wa kujitegemea kuanzia mwaka 1969.

Aliwahi kuwa Rais wa Uganda kwa muda na mwansheria mkuu baada ya nchi hiyo kupata uhuru miaka ya 60.

Baada ya Idi Amin kuchukua madaraka mwaka 1971, alikwenda uhamishoni Marekani, ambapo alifanya kazi kama mwanasheria huko Mount Vernon, mjini New York.

Wakati alipokuwa Marekani, alikuwa mwanachama wa Uganda Freedom Union, moja miongoni mwa makundi yaliyokuwa yakimpinga Amin uhamishoni.

Kufuatia kupinduliwa kwa Idi Amin mwaka 1979, Binaisa akarejea Uganda. Baada ya Idi Amin, Yusuf Lule, ndiye alikuwa Rais wa mpito kwa siku 68.

Juni 20, 1979, Binaisa aliteuliwa kuwa Rais wa Uganda na baraza tawala la wakati huo la National Consultative Council- NCC, chombo kilichokuwa chini ya Uganda National Liberation Front (UNLF), muungano wa waliokuwa uhamishoni kutoka Uganda waliosaidia kumwondoa Idi Amin.

Binaisa alipinduliwa Mei 12, 1980 na tume ya jeshi, chombo chenye nguvu cha UNLF kilichokuwa kinaongozwa na Paulo Muwanga, na ambapo naibu wake alikuwa Yoweri Museveni (wakati huo akiwa kiongozi wa Uganda Patriotic Movement).

Nchi hiyo baada ya hapo ikawa inaongozwa na tume ya Rais ya Uganda (iliyoundwa siku chache baada ya mapinduzi hayo) wakiwemo Paulo Muwanga, Yoweri Museveni, Oyite Ojik na Tito Okello.

Tume hiyo ya Rais iliiongoza Uganda mpaka uchaguzi mkuu wa Rais wa Desemba 1980.

Binaisa alijiunga, na akateuliwa kuwa naibu waziri wa Uganda Patriotic Movement.

Ushindi ulipatikana kupitia chama cha Millton Obote cha Uganda Peoples Congress, hata hivyo, matokeo hayo yalipingwa, na kusababisha Museveni kuanzisha uasi msituni, uliosababisha yeye kupata urais tangu mwaka 1986.