Afrika Kusini yafafanua hatua ya kumwita balozi wake wa Rwanda

Gen Nyamwasa
Image caption Gen Nyamwasa

Msemaji katika wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini, ameielezea hatua ya nchi yake ya kumwita nyumbani balozi wake wa nchini Rwanda kuwa "hatua ya kawaida ya kidiplomasia".

Siku ya Alhamis utawala mjini Pretoria ilimwita balozi wake kwa mashauriano kufuatia tukio la mwezi June la kupigwa risasi kwa afisa wa kijeshi wa Rwanda, anayeishi uhamishoni mjini Johannesburg, Generali Faustin Kayumba Nyamwasa.

Msemaji huyo, Saul Molobi, ameiambia BBC kuwa uamuzi huo ulichukuliwa kwa ajli ya kutathimini hali ya usalama ya Afrika Kusini kwa ujumla, na wala haihusiani na tukio la kupigwa risasi kwa Gen Nyamwasa pekee.

Hata hivyo, Bw Molobi, aliongeza kuwa wakati uhusiano kati ya nchi yake na Rwanda ukiwa imara, Pretoria haifurahii kuhusu baadhi ya mambo ambayo hakutaka kuyafafanua.

Inaaminika kuwa Afrika Kusini imechukua hatua ya kumwita nyumbani balozi wake nchini Rwanda, kufuatia mzozo wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili, kuhusu kujeruhiwa kwa Gen Nyamwasa.