Uhesabuji kura waanza Rwanda

Image caption Upigaji kura Rwanda

Shughuli za upigaji kura zimekamilika nchini Rwanda na uhesbauji kura umeshaanza.

Rais Paul Kagame kutoka chama cha RPF anapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi na ametangaza kuridhishwa na mchakato mzima licha ya kuwepo shutma za kuwakandamiza upinzani.

Wananchi zaidi ya milioni tano wa Rwanda wameamkia kwenye vituo vya kupigia kura kumchagua rais atakayewaongoza kwa muhula wa miaka saba ijayo.

Uchaguzi huu wa pili kufanyika tangu Rwanda kukumbwa na mauaji ya kimbari mwaka 1994 umeelezwa kufanyika kwa hali ya utulivu na kuitikiwa na idadi kubwa ya wapiga kura.

Kagame apewa nafasi kubwa ya ushindi

Misururu mirefu ya wapiga kura ilionekana kwenye vituo vya kupigia kura tangu asubuhi lakini hadi saa nne sehemu kadhaa za nchi zilishakamilisha shughuli yenyewe kama alivyofahamisha mkuu wa tume ya uchaguzi.

Image caption Upigaji kura Rwanda

Rais Paul Kagame alipigia kura kwenye kituo cha Rugunga mjini na baada ya kupiga kura alitangaza kuridhika na kiwango cha demokrasia ambacho Rwanda imefikia.

Alisema mchakato mzima wa uchaguzi umeonyesha kuwa Wanyarwanda wamekomaa katika swala la demokrasia.

Rais Kagame anapewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi wa uchaguzi huu kama ilivyotokea mwaka 2003.

Alisema yuko tayari kukubali matokeo na ana mengine ya kufanya iwapo atashindwa kwenye uchaguzi huu.

Upinzani

Wagombea wengine wanaochuana na Rais Kagame kwenye uchaguzi huu ni pamoja na Dr Jean Damascene Ntawukuriryayo kutoka chama cha Social Democratic, Dr Alivera Mukabaramba wa chama cha maendeleo na mshikamano na Prosper Higiro kutoka Liberal Party.

Wote wamepiga kura kwenye maeneo tofauti. Bwana Higiro baada ya kupiga kura yake aliunga mkono kauli ya kwamba uchaguzi huu unabainisha Rwanda imepiga hatua kubwa ya demokrasia kwa kushirikisha wagombea wengi.

Kulingana na tume ya taifa ya uchaguzi, shughuli zote zimekwenda uzuri kama ilivyopangwa na hakuna dosari ama malalamiko kutoka vyama vingine.

Tume hiyo imesema matokeo ya muda yatatolewa tarehe 11 na matokeo rasmi kutangazwa kabla ya tarehe 17 mwezi huu wa Agosti.