Watu wafa kwa kuzama Ziwa Tanganyika

Image caption Ramani ya Kongo kuonyesha eneo la Kivu.

Takriban watu 50 wamekufa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia katika Ziwa Tanganyika, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, watu walikuwa wakisafiri pamoja na bidhaa walizokusudia kuziuza kuelekea jimbo la kusini la Kivu karibu na mpaka na Burundi.

Mwandishi wa BBC, Lubunga Byaombe, anasema watu 19 walinusurika ajali hiyo.

Ajali za barabarani ni jambo la kawaida katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa sababu ya uendeshaji mbaya, magari machakavu na barabara mbovu.

Mnamo mwezi uliopita takriban watu 220 walikufa baada ya gari la kubebea mafuta kupinduka na kulipuka katika kijiji cha Sange, Kivu Kusini.