Joe Cole afungiwa mechi tatu

Mchezaji kiungo wa Liverpool Joe Cole atakosa kucheza mechi tatu baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika pambano lake la kwanza kwa niaba ya Liverpool ambalo lilimalizika kwa sare ya 1-1 siku ya Jumapili.

Cole mwenye umri wa miaka 28 alipewa adhabu hiyo kwa kumpiga ngwara Laurent Koscielny na hatacheza mechi dhidi ya Manchester City, West Bromwich Albion na Birmingham.

Image caption Joe Cole, Liverpool

Liverpool iliamua kutokata rufani kwa kadi hiyo nyekundu na kocha Roy Hodgson alisema baada ya kuchunguza video ya mechi hiyo wameona kwamba ilikua ni bahati mbaya kwa Cole na kwamba hakukusudia kucheza rafu.

Wakati huo huo Kocha Hodgson amekataa kumlaumu mlinda lango Pepe Reina kwa makosa yake ambayo yaliiruhusu Arsenal kutoka sare na Liverpool katika uwanja wa Anfield.

Amesema Pepe Reina amevunjika moyo sana hasa kwa kuwa amecheza vizuri sana ukichukulia kwamba anasumbuliwa na maumivu ya bega.

Makosa ya Reina yaliisaidia Arsenal kukomboa sare dhidi ya Liverpool.

David Ngog alifungua mlango kwa Liverpool mara baada ya kipindi cha pili. Lakini matumaini ya Liverpool kujipatia ushindi yalififia katika dakika ya mwisho kutokana na cross ya Marouane Chamakh ambayo Reina aliitema na kuiskumiza kimiani.

Katika mechi hiyo hiyo Koscielny wa Arsenal alitolewa nje na mwamuzi baada ya kuonyeshwa kadi yake ya pili ya njano alipounawa mpira .