Mkenya aliyemwuuza albino afungwa

Mahakama nchini Tanzania imemhukumu raia mmoja wa Kenya anayedaiwa kumwuuza albino kifungo cha miaka 17 gerezani na kutozwa faini ya zaidi ya dola za kimarekani 50,000.

Mahakama hiyo imemhukumu Nathan Mutei baada ya kukiri kosa la kumwuuza binadamu.

Image caption Mama albino akiwa mjini Dar es Salaam

Polisi walisema walimkamata Mutei alipojaribu kumwuuza mwenzake kutoka Kenya ambaye ni albino kwa kiwango cha karibu zaidi ya dola za kimarekani 250,000.

Viungo vya albino vina thamani katika maeneo kadhaa ya Afrika, huku waganga wa kienyeji wakidai kuwa vina faida za kipekee.

Mwandishi wa BBC nchini Tanzania Eric Nampesya alisema, albino huyo, Robinson Mkwama, anasindikizwa nyumbani Kenya na polisi.

Mutei, mwenye umri wa miaka 28, alikamtwa nje tu ya mkoa wa Mwanza.

Katika harakati hizo za kumkamata, iliyotangazwa rasmi siku ya Jumanne, polisi walijiweka katika nafasi ya wafanyabiashara wanaonunua viungo vya albino.

Kamanda polisi wa mkoa huo, Simon Siro, aliiambia BBC Bw Mutei alimlaghai Bw Mkwama, mwenye umri wa miaka 20, kuwa atapata kazi Tanzania kama msaidizi wa dereva la lori.

Nchini Tanzania, viungo vya maalbino hutumiwa na waganga wa kienyeji kutengeneza dawa wanazowaambia wateja wao zitawasaidia kuwa matajiri au kuwa na afya njema.

Idadi kadhaa ya maalbino wameuawa, na mauaji hayo yameenea mpaka nchi jirani ya Burundi.

Serikali ya Tanzania imeahidi kuwasaka wanaouza viungo vya albino, na wengi wamehukumiwa kifo kufuatia mauaji hayo.