Nasri kutocheza kwa mwezi mzima

Klabu ya Arsenal imepigwa na bumbuazi kufuatia habari za kuwa mcheza kiungo wake wa kutegemewa Samir Nasri hatoshiriki mechi yoyote kwa kipindi cha mwezi mzima kutokana na tatizo la goti.

Klabu hiyo ilianza msimu mpya wa Ligi kuu kwa kutoka sare ya bao moja dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili.

Image caption Samir Nasri, kushoto

Timu iliyoshiriki mechi hiyo ilitegemea mno huduma za mcheza kiungo huyo aliyeshikilia nafasi ambayo kwa kawaida huwa ya nahodha Cesc Fabregas.

Sasa inasemekana kuwa hatoshiriki hadi mechi tano za Ligi ya England ikiwa ni pamoja na michuano ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya itakayoanza katikati ya mwezi Septemba.

Taarifa kutoka klabu ya Arsenal imesema kuwa mchezaji huyo atafanyiwa upasuaji leo kufuatia jeraha alilopata wakati wa mchuano kati ya Liverpool na Arsenal kwenye uwanja wa Anfield.

Taarifa hiyo imeongezea kusema kuwa, Nasri ambaye amekuwa katika hali nzuri ya afya na matarajio ya kufanya vyema msimu huu atakaa nje ya mashindano kwa takriban mwezi mzima.