Risasi za plastiki zafyatuliwa A Kusini

Image caption Mgomo Afrika Kusini

Polisi wa Afrika Kusini wamefyatua risasi za plastiki na kuumwagia maji mkusanyiko wa wafanyakazi wa serikali wanaoandamana nje ya hospitali mjini Soweto.

Zaidi ya wafanyakazi wa umma milioni moja wameanza mgomo siku ya Jumatano wakitoa wito wa kuongezewa mishahara.

Jumuiya nyingine za wafanyakazi zimejiunga katika mgomo huo ambapo ni siku ya pili.

Wakati huo huo, mamlaka za afya huko Guateng zimesema wataalamu wa tiba wa kijeshi wamepelekwa ili kusaidia katika baadhi ya hospitali kutokana na upungufu wa wafanyakazi.

Waziri wa afya wa jimbo hilo alisema pia wanachunguza vifo vya watu watano vilivyotokea usiku hospitalini mashariki mwa Johannesburg kama vina uhusiano na upungufu wa wafanyakazi kutokana na mgomo.

Mashirika hayo yaliyo na ushirikiano na Cosatu, shirikisho kuu la wafanyakazi wa Afrika Kusini, yamekuwa yakitaka ongezeko la mshahara kwa asilimia 8.6.

Lakini serikali ya Afrika Kusini imesema haina uwezo wa hata asilimia saba iliyoahidi kuwapa polisi, walimu, madaktari na wauguzi.

Helikopta kuzungukazunguka

Wafanyakazi hao waliogoma huko Soweto huku wakipiga makelele waliwazuia wagonjwa kuingia hospitali siku ya Alhamis asubuhi, polisi, ambao kisheria wanapigwa marufuku kugoma, wakaingia kusaidia wagonjwa.

Msemaji wa polisi Kapteni Nondumiso Mpantsha alisema waandamanaji hao pia walijaribu kutumia nguvu kuwapita askari doria ndani ya hospitali ya Chris Hani Baragwanath.

Alisema, " Hali kwa sasa ni shwari kwasababu kuna polisi wengi wamesambazwa eneo hilo."

Jumuiya hizo za wafanyakazi pia zinapanga kufunga moja ya barabara kuu mjini Johannesburg siku ya Alhamis.

Walimu wametishia kuvuruga masomo katika shule binafsi.