"Tuko na Pakistan" wasema wafadhili

Hali ya kibinadamu nchini Pakistan imeelezewa kuwa mbaya sana
Image caption Hali ya kibinadamu nchini Pakistan imeelezewa kuwa mbaya sana

Jumuiya ya kimataifa imeahidi kutoa fedha zaidi kwa Pakistan ambayo imekumbwa na mafuriko mabaya sana, katika mkutano wa dharura wa kikao kikuu cha Umoja wa Mataifa.

Waziri wa masuala ya kigeni wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi amesema amehakikishiwa kwamba kiwango cha fedha kilicho pendekezwa na Umoja huo cha dola milioni 460 kitafikiwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kuwa mafuriko hayo yanaweza kulinganishwa na kimbunga cha tsunami ambacho kinaenda kwa mwendo wa pole.

Yamkini watu milioni ishirini wameathirika na wataalam wanasema misaada ya vyakula, maji safi na mahema inatakikana haraka ili kuepuka janga kubwa la kibanadamu.

Kabla ya mkutano huo kuanza Ban Ki-moon alisema kwamba misaada haikuwa imefikia nusu ya kiwango cha fedha ambacho kilikuwa kimelengwa. Dola milioni 460 zinahitajika kuijenga upya nchi hiyo lakini hadi sasa wafadhili hawajajitokeza vilivyo kuchangia misaada kwa nchi hiyo.

Marekani ambayo hadi sasa imetoa fedha zaidi kwa mfuko wa misaada imetangaza kwamba itatoa dola milioni 60 zaidi na kufikisha idadi ya mchango wake kwa Pakistan kuwa dola milioni 150.

Waziri wa masuala ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton amesema kuwa dola milioni 92 zitatolewa kwa mfuko huo wa Umoja wa Mataifa.