Marekani yataka Al-Megrahi akamatwe tena

Al-Megrahi
Image caption Al-Megrahi

Mshauri wa Rais Obama anayehusika na masuala ya kupambana na ugaidi ametoa wito wa kurejeshwa jela huko Scotland kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kulipua ndege mjini Lockerbie mwaka wa 1988.

John Brennan alisema hatua ya serikali ya Scotland ya kumwachiliwa huru Abdelbaset al Megrahi, raia wa Libya haikuwa sahihi.

Bw Brennan alisema mtu huyo alipatikana na hatia ya kuhusika na ugaidi na anapaswa kukamilisha kifungo cha miaka 27.

Bw Megrahi aliachiliwa huru mwaka mmoja uliopita baada ya madaktari kuthibitisha kuwa anaugua saratani isiyokuwa na tiba.

Al-Megrahi aliyekuwa afisa wa ujasusi wa Libya ndiye mtu pekee aliyehukumiwa kwa ulipuaji wa ndege ya shirika la ndege la Pan Am iliyodunguliwa kwenye anga za Lockerbie, Uskochi na kuwauwa watu mia mbili na sabini mwaka 1988.

Wengi wa waathirika walikuwa raia wa Marekani.

Maseneta wa Marekani wanataka kupewa maelezo zaidi kuhusu ushauri wa kimatibabu uliowezesha kuachiliwa kwa Al- Megrahi.

Wametaka pia kupewa mawasiliano yaliyotokea kati ya serikali ya Uingereza na kampuni ya mafuta ya BP ya Uingereza ambayo ilihusika katika mashauriano na Libya wakati wa kuachiliwa kwa Al-Megrahi.