Wananchi Niger wataabika kwa majanga

Image caption Kumekuwa na matatizo mengi kwa wakati mmoja na kufanya serikali ishindwe kusaidia wananchi kikamilifu.

Ukame, mafuriko na kupanda kwa bei ya chakula ni matatizo yaliyowaacha mamilioni ya raia wa Niger katika hali ya kutapatapa wakati kipindi cha mavuno yakisubiriwa miezi kadhaa.

Mfanyakazi wa shirika la misaada la nchini Niger amejitolea kusaidia wanakijiji cha Tidirra, kilichoko kusini mwa nchi.

Akitokwa jasho la jua kali ndani ya nyumba iliyojengwa kwa matofali ya udongo, Adamo Gabeye anachanganya unga wenye rangi ya dhahabu hivi na sehemu ndogo ya ufuta na vitamini.

Kwa utaratibu unaoelekea kama anayetayarisha mkate, Gabeye anachanganya ufuta na unga wa mahindi, soya na sukari.

Anayafanya hayo huku akiandamwa na akina mama 14 waliokalia viti upande mmoja wa chumba.

Vitoto vichanga vilivyopakatiwa na mama hawa vinahangaika kutafuta maziwa ingawa akina mama hawana tena uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha. Hali hii inatishia watoto hawa wanaoonekana kama wenye upungufu mwilini.

Takwimu

Hiyo ndiyo hali iliyoko Niger mojawapo ya nchi masikini duniani, lakini kwa sasa inakabiliwa na kukosa chakula.

Mvua ya kupindukia katika sehemu za nchi mwaka uliopita iliharibu mashamba na mazao kama mawele, mtama na mahindi ikisababisha upungufu mkubwa wa mavuno na hadi mwaka huu watu wamekosa chakula.

Zaidi ya asilimia 80 ya watu wa Niger, takriban watu milioni 12 wanakabiliwa na ukosefu wa chakula. Utapia mlo ni wa kupindukia na hali hiyo imezidi viwango vya dharura.

Bei ya chakula yapanda

Serikali ya Niger imeyahimiza mashirika ya kimataifa ya misaada yanunue chakula nje ya nchi ili kuepusha kupanda kwa bei katika masoko ya ndani.

Hakuna anayekanusha kupanda kwa bei ya chakula nchini Niger. Bei ya mawele ilipanda mara dufu katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa serikali, wafanyabiashara wakubwa wameshikilia biashara ya kuagiza chakula kutoka nje na hivyo kupandisha bei wanavyotaka.

Na katika chumba anakochanganya unga wenye rangi ya dhahabu na soya, ufuta na sukari Adamo anafahamu vyema kuwa watoto waliomkodolea macho watategemea mchanganyiko wa ugali anaoutengeneza ili kunusuru maisha yao.