Liverpool yamsajili Raul Meireles

raul meireles
Image caption raul meireles

Klabu ya Liverpool imeimarisha sehemu ya kiungo baada ya kufanikiwa kumsajili Raul Meireles kutoka Porto ya Ureno.

Liverpool imelipa euro milioni 14 sawa na paundi milioni 11.5 za Uingereza kuweza kumnasa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 27 aliyekwishacheza mechi 38 za kimataifa.

Mchezaji huyo mwenye nguvu sehemu ya kiungo anaonekana ataziba ipasavyo pengo lililoachwa na Javier Mascherano anayekamilisha harakati za kuhamia Barcelena.

Meireles amesema meneja wa Liverpool Roy Hodgson amefanya kazi kubwa kuweza kumsajili na kwake ni hiyo historia kubwa kujiunga na Liverpool.

Ameeendelea kusema ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi kucheza ligi ya England na sasa ndoto hiyo imetimia.

Meireles anaungana na akina Milan Jovanovic, Joe Cole, Christian Poulsen, Jonjo Shelvey na Danny Wilson waliojiunga na Liverpool msimu huu.

Kiungo huyo aliichezea Ureno mechi zote nne nchini Afrika Kusini katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.

Katika miaka yake sita aliyoichezea Porto mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Boavista na Aves amefanikiwa kushinda mara nne ubingwa wa ligi ya Ureno.