Semenya achaguliwa kushiriki Madola

Bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 kwa wanawake Caster Semenya ameteuliwa katika kikosi cha Afrika Kusini kitakachoshirki mashindano ya Jumuia ya Madola.

Image caption Caster Semenya

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 19 alirejea uwanjani mwezi wa Julai baada ya kuwa nje kwa kipindi cha miezi 11 kufuatia utata uliojitokeza juu ya jinsia yake na ameshinda ameshinda mara tatu baada ya kurejea.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shirikisho la Olympic la Afrika Kusini Gideon Sam, wamefurahishwa sana na kurejea kwa Semenya na kwamba ataweka jitahada zake katika kushinda mashindano hayo.

Mashindano hayo yatafanyika katika mji mkuu wa India, New Delhi kuanzia tarehe 3- 14 mwezi wa Oktoba.

Semenya alihana hatia na tuhuma kwamba jinsia yake ina utata na kuruhusiwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) lililomfungia, baada ya kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya riadha ya dunia mwaka jana na baadae kufanyiwa vipimo vya mkojo kubaini kama ni mwanaume au mwanamke.

Licha ya kukosa mashindano ya ubingwa wa Afrika mwishoni mwa mwezi wa Julai, alirejea mashindano kushiriki mashindano ya Ulaya na kushinda nchini Finland na Ujerumani.

Alishinda mjini Berlin mbio za mita 800 siku ya Jumapili kwa kutumia muda wa dakima moja sekunde 59.90 na ingawa muda huo haukuwa mzuri wa dakika moja sekunde 55.45 aliouweka kushinda ubingwa wa dunia mwaka jana, bado Semenya anapewa nafasi ya kushinda medali ya dhahabu huko India.