Sibanda wa MDC Zimbabwe afariki dunia

Gibson Sibanda wa Zimbabwe
Image caption Gibson Sibanda wa Zimbabwe

Mwanzilishi mwenza wa iliyokuwa chama cha upinzani cha Zimbabwe, the Movement for Democratic Change, amefariki dunia akiwa ana umri wa miaka 66.

Gibson Sibanda alikuwa kiongozi maarufu wa chama cha wafanyakazi kabla ya uhuru wa Zimbabwe mwaka 1980 na alikamatwa mara kwa mara kutokana na harakati zake.

Alisaidia kuunda chama cha MDC mwaka 2000 lakini alijiengua miaka mitano baadae baada ya kuibuka tofauti baina yake na Morgan Tsvangirai.

Bw Sibanda alijiunga na sehemu ya chama cha MDC iliyokuwa imejitenga na wakati kifo chake kilipotokea alikuwa waziri wa serikali ya muungano.

Msemaji wa chama chake alisema Bw Sibanda alikuwa akiugua saratani kwa muda sasa na alikufa huko Bulawayo.

Bw Sibanda na Bw Tsvangirai wote walikuwa viongozi wa chama cha wafanyakazi walipoamua kuunda MDC kupambana kwa kile walichosema sera mbovu za kiuchumi za Rais Robert Mugabe.

Bw Tsvangirai ni waziri mkuu wa serikali ya kugawana madaraka ya sasa iliyoundwa miezi 18 iliyopita.

Serikali hiyo inajaribu kuimarisha uchumi uliotikiswa na mfumko mkubwa wa bei na upungufu wa chakula pamoja na mafuta.