Mapigano yaendelea mji mkuu wa Somalia

Askari wa jeshi la Somalia
Image caption Askari wa jeshi la Somalia

Mapigano makali yanaendelea kwa siku ya sita kati ya jeshi la serikali na waasi wa kiislam katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Maafisa wa hospitali wanasema takriban watu mia moja wameuwawa na wengine mia mbili na ishirini kujeruhiwa tangu waasi wakiislam kuanzisha upya vita dhidi ya serikali mwanzoni mwa wiki hii.

Maelfu ya watu wanaukimbia mji mkuu wakati waasi wakijaribu kuiteka barabara muhimu inayounganisha ikulu ya rais na uwanja wa ndege.

Mwandishi wa BBC mjini Mogadishu amesema waasi wa kiislam wako umbali wa nusu kilometer tu kuifikia barabara hiyo, ambayo ndiyo pekee inayotumiwa na serikali kwa sasa.

Al-Shabab ilianza mapigano siku ya Jumatatu baada ya msemaji wake kutangaza kuandaa "vita vikubwa" dhidi ya majeshi ya AU, wakiwaelezea wanajeshi hao wa kutunza amani 6,000 kama "wavamizi".

Siku ya Jumanne Al-Shabab ilidai kuhusika na uvamizi wa hoteli iliyopo karibu na kasri ya Rais na kuua wabunge sita watu wengine zaidi ya thelathini.