Rwanda kufikiria uhusiano wake na UN

Wakimbizi wa Rwanda
Image caption Wakimbizi wa Rwanda

Rwanda imesema itafikiria kuendelea na ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa, haswa katika masuala ya kulinda amani--ikiwa repoti inayokosoa vikali jeshi la Rwanda itachapishwa.

Repoti hiyo, ambayo inajumuisha matukio kuanzia mwaka wa 1993 hadi mwaka wa 2003, inasema wanajeshi wa Rwanda huenda wamehusika na mauaji ya kimbari wakati wa mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Waziri wa sheria wa Rwanda, Tharcisse Karugarama, alisema Umoja wa wa Mataifa uliichoma kisu mgongoni Rwanda na haupaswi kuchapisha repoti hiyo isiyokuwa na ukweli wowote.

Rwanda inachangia maelfu ya wanajeshi katika kikosi cha kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan.

Ripoti hiyo, iliyosomwa na BBC inasema kuwa maelfu ya Wahutu wakiwemo wanawake, watoto na wazee waliuawa na Jeshi la Rwanda lenye askari wengi wa kabila la Kitutsi.

Ripoti hiyo vile vile inaorodhesha ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na vikosi vya nchi nyingine zilizoshiriki kilichokuja kujulikana kama ''Vita vya kwanza vya Afrika''.

Ripoti kamili ya shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa itachapishwa hivi karibuni. Ingawaje mgogoro huo umemalizika rasmi, hali katika eneo la mashariki mwa Congo lililopakana na Rwanda bado ni ya wasiwasi.

Ripoti hiyo yenye kurasa 545, iliyotayarishwa na maofisa 20 wa shirika la haki za binadamu, inaorodhesha kilichoitwa mashambulio yaliyopangwa na kutekelezwa na jeshi la Rwanda pamoja na waasi wa AFDL.