Aliyecheza Kombe la Dunia 1930 afariki

Francisco Varallo
Image caption FranciscoVarallo

Mchezaji wa soka pekee aliyekuwa hai miongoni mwa wachezaji waliocheza fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia mwaka 1930, Francisco Varallo wa Argentina, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.

Varallo alicheza katika mchezo wa fainali kati ya Uruguay na Argentina mjini Montevideo, Uruguay mwaka 1930.

Timu yake ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 4-2 na Uruguay.

Varallo wakati akiichezea klabu yake ya Boca Juniors aliweza kupachika mabao 194, ikiwa ni rekodi ya timu hiyo ambayo ilivunjwa mwaka huu na mchezaji wa timu hiyo Martin Palermo.

Jina lake la utani alikuwa akiitwa"Canoncito" kutokana na uwezo wa kufyatua mashuti makali.

Alipohojiwa na FIFA wakati wa kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwake mwaka huu, Varallo alisema tukio baya zaidi ambalo analikumbuka hadi sasa ni pale walipofungwa na Uruguay mwaka 1930.

"Nililia siku ile. Na hadi sasa ninapokumbuka bado najisikia hasira" alisema Varallo.

Varallo alistaafu kucheza soka baada ya kuumia alipokuwa na umri wa miaka 30 na akawa ni kocha wa timu za daraja la chini za Boca na pia klabu ya Gimnasia.