Spurs yasubiri kumsajili Van der Vaart

Rafael Van der Vaart
Image caption Rafael Van der Vaart

Tottenham inatarajia kufahamu Jumatano hii, iwapo wasimamizi wa Ligi Kuu ya England wataidhinisha mipango yao ya kumsajili kiungo Rafael Van der Vaart.

Spurs imemsajili kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 kutoka klabu ya Real Madrid zikiwa zimesalia saa mbili kabla ya muda wa usajili kufungwa saa kumi na mbili jioni siku ya Jumanne.

Wasimamizi wa Ligi Kuu ya England hivi sasa wanaangalia iwapo usajili huo ulifanywa kwa wakati na wanazungumza na klabu zote mbili zinazohusika.

Meneja wa Tottenham Harry Redknapp, amesema"Nilipofika siku ya Jumanne asubuhi halikuwa jambo nililokuwa nimepanga kulifanya".

"Ilikuwa ni kazi ya dakika za mwisho. Nadhani awali alikuwa akielekea Bayern Munich siku ya Jumatatu kwa dau la paundi milioni 18 na ghafla bei yake ikaporomoka.

Nilifahamishwa saa kumi jioni kwamba anaweza kusajiliwa kwa paundi milioni 8 na kwa fedha hizo na kwa vile ni mchezaji hodari na hapana shaka atatusaidia, ndio tumeamua kumchukua.

Wasimamizi wa Ligi Kuu ya England wanataka kuhakikisha iwapo mkataba umefanyika mapema kabla ya muda wa mwisho uliowekwa na ikiwa ni hivyo, basi wataruhusu mkataba ukamilishwe.