Waandamanaji wafariki dunia Msumbiji

Image caption Maandamano Msumbiji

Imearifiwa kuwa watu sita wameuawa kufuatia maandamano mjini Maputo nchini Msumbiji juu ya kupanda kwa bei ya chakula na mafuta.

Polisi imethibitisha vifo vya watoto wawili na kusema kuwa ghasia zimeenea katika maeneo mbalimbali ya mji.

Waandamanaji waliwarushia mawe maofisa wa polisi na kuweka vizuizi barabarani.

Awali serikali ilionya kuwa maandamano hayatovumiliwa.

'Ghadhabu'

Televisheni binafsi ya Msumbiji ijulikanayo kama S-TV pamoja na shirika la habari la Ureno, Lusa vimeripoti watu sita kuuawa katika maandamano yaliyofanywa Jumatano katika mji mkuu.

Shirika la Lusa limenukuu duru za hospitali zikielezea kuwa jumla ya watu 11 wamejeruhiwa ingawa polisi imethibitisha vifo vya watu wawili.

Msemaji wa polisi Arnaldo Chefo alisema kwenye taarifa yake, "Watu kadhaa wamejeruhiwa. Watoto wawili wamefariki katika kitongoji cha Mafalala. Kuna hali ya mtafaruku na fujo sehemu mbalimbali za mji mkuu.

Maduka yamefungwa na usafiri wa umma umekwama kufuatia maandamano hayo.

Mkaazi mmoja wa mji mkuu Maputo, Nelfa Temoteo, alisema "Nimeshindwa kujinunulia chakula changu binafsi kutokana na bei ghali ya chakula, nimeghadhabishwa na kupanda huku kwa hali ya maisha."

Raia wa Msumbiji wamejionea bei ya mkate mmoja ukipanda kwa asilimia 25 wakati thamani ya sarafu ya nchi hiyo Metical ikishuka kulinganisha na Rand ya Afrika ya kusini.

Bei ya petroli na maji pia vimepanda.

Mwaka 2008, mapambano baina ya polisi na waandamanaji yalisababisha vifo vya watu wanne na wengine 100 kujeruhiwa.

Maandamano ya wakati huo yaliichagiza serikali kuahirisha mipango yake ya kupandisha bei ya mafuta ya petroli.