A Kusini yalaani hukumu ya Ravalomanana

Afrika Kusini imeikosoa vikali Madagascar kwa kutoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kilichotolewa kwa Rais Marc Ravalomanana anayeishi uhamishoni.

Waziri wa mahusiano ya kimataifa na ushirikiano Maite Nkoana-Mashabane alisema hukumu za aina hizo hazitosaidia kumaliza machafuko ya kisiasa huko Madagscar.

Image caption Marc Ravalomanana

Bw Ravalomanana yuko uhamishoni Afrika kusini baada ya kupinduliwa Machi 2009.

Alihukumiwa kutokana na mauaji ya takriban watu 30 wakati wa maandamano.

Waliofariki dunia ni wafuasi wa Andry Rajoelina, aliyeingia madarakani huku akiungwa mkono na jeshi la nchi hiyo baada ya Bw Ravalomanana kukimbia.

Serikali ya Bw Rajoelina haitambuliki kimataifa na Afrika kusini inaongoza jitihada za kumaliza ghasia hizo za kisiasa.

Bi Nkoana-Mashabane alisema uamuzi wa jaji huenda umetokana na ushawishi wa kisiasa.

Alisema, " Sidhani kama hukumu zinazotolewa huku mshtakiwa akiwa hayupo zinasaidia kutatua matatizo Madagascar."

Mawakili wa upande wa utetezi wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo waliondoka muda mfupi baada ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, wakisema mahakama hiyo ilikuwa ikitumiwa na utawala wa Rajoelina.

Wakili Hanitra Razafimanantsoa ameliambia shirika la habari la AFP, " Nia ni kumhukumu ili asiweze kurudi Madagascar na kugombea urais siku za usoni."

Madagascar imekuwa katika mgogoro wa kisiasa kwa kipindi cha miaka 19 iliyopita.

Hii ni hukumu ya tatu kutolewa na mahakama tangu Bw Ravalomanana kuondoka nchini humo.