Wengi wakamatwa kwa vurugu Msumbiji

Polisi nchini Msumbiji inawashikilia watu 142 kwa kuhusika na vurugu zilizosababisha vifo vya watu 10.

Kupanda kwa bei ya mkate na bidhaa nyingine kulizusha siku tatu za maandamano kwenye mitaa ya mji mkuu Maputo.

Image caption Ghasia Msumbiji

Wengine sita wamewekwa mbaroni wakishukiwa kuhamasisha ghasia kaskazini mwa jimbo la Nampula.

Serikali ya Msumbiji imekataa wito wa kuchukua hatua za kupunguza bei ya mkate ikisema kupanda huko kwa bei ‘hakuzuiliki.’

Bei za mafuta ya petrol na umeme pia zimepanda.

Kumekuwa na ujumbe mfupi wa simu ukisambazwa kuwataka watu kuendelea na ghasia.

Kuna baadhi ya taarifa kuwa watu sita waliowekwa kizuizini na polisi mjini Nampula wanashukiwa kusambaza ujumbe mfupi wa simu.

Lakini msemaji wa polisi katika eneo hilo Inacio Dina amekanusha taarifa hizo na kusema kuwa walikuwa wakihamasisha mkutano wa kupanga ghasia.

Mmoja kati ya wanaoshikiliwa na polisi hata hivyo alisema mkutano huo ulikuwa wa chama cha upinzani cha Renamo.

Jumatatu mji wa Maputo uliripotiwa kuwa tulivu lakini ukiwa na idadi kubwa ya polisi katika vitongoji vyake hasa eneo vurugu zilikoanzia.

Watu wapatao 443 wamejeruhiwa tangu vurugu hizo zianze, waziri wa afya Ivo Garrido alisema Ijumaa.

Kulizuka mapigano pia katikati mwa mji wa Chimoio.

Kupanda kwa bei kumesabishwa na kushuka kwa thamani ya fedha ya Msumbiji dhidi ya Randi ya Afrika Kusini, wachambuzi wanasema.

Lakini pia kumesababishwa na kupanda kwa bei ya ngano duniani kufuatia ukame ulioikumba Urusi, moja ya nchi zinazouza ngano kwa wingi nje.