Bei ya mkate yapunguzwa Msumbiji

Image caption Msumbiji

Msumbiji itabadilisha ongezeko la bei ya mikate iliyosababisha kuibuka kwa ghasia wiki iliyopita.

Tangazo la kubadilisha sera zimetolewa na waziri wa mipango, Aiuba Cuereneia, ambaye amesema pia kwamba nchi hiyo itarejesha baadhi ya ruzuku ya umeme na maji.

Ongezeko la bei ya vyakula na bidhaa nyingine zilisababisha maandamano ya siku tatu.

Serikali ilisema zaidi ya watu 400 walikamatwa wakati wa maandamano hayo, iliyosababisha watu 13 kufariki dunia.

Taarifa ya waziri ilisema kwamba serikali " itaendelea kuuza mkate kwa bei ya awali huku wakipanga ruzuku."

Awali serikali ya Msumbiji ilisema ongezeko la bei "haibadiliki".

Kuweka bei ndogo ya bidhaa nchini humo ni ngumu kwani kiwango kikubwa cha chakula chao hutoka nchi za nje.

Taifa hilo lililopo kusini mashariki mwa bara la Afrika linazalisha asilimia 30 tu ya ngano inayohitaji.

Ongezeko kubwa la bei ya vyakula lilisababishwa kwa upande mmoja na thamani ya pesa ya Msumbiji dhidi ya randi ya Afrika Kusini, ambapo wachambuzi wanasema bidhaa kutoka nje zinazidi kuwa ghali.

Pamoja na hayo, bei ya ngano imeongezeka kufuatia ukame nchini Urusi, muuzaji mkuu wa ngano duniani.