Umoja wa mataifa uliwakosea wanawake na watoto DRC

Image caption Mwanamke mwathiriwa wa ubakaji DRC

Afisaa mmoja mkuu wa umoja wa mataifa ameelezea kuwa wanajeshi wa umoja wa mataifa wamekosa kuwalinda wanawake na watoto waathiriwa wa ubakaji, katika eneo la mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokerasia ya Congo.

Kwa mujibu wa afisaa huyo aliyewahoji baadhi ya waathiriwa, wengi walikosa kulindwa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Afisaa huyo Atul Khare alifahamisha baraza la usalama la umoja huo kwamba idadi ya walioathirika na visa vya ubakaji inakadiriwa kufikia miatano. Alifahamisha BBC kwamba wanajeshi hao walijikokota katika kuchukua hatua za kuwalinda wanawake na watoto hasa kwa sababu hawakutambua kwa haraka masaibu yaliyokuwa yanawakumba waathiriwa.

Aliongeza kuwa hatua kadhaa tayari zimechukuliwa kurekebisha hali ingawa aliomba msaada zaidi wa kimataifa kuhakikisha kuwa hali hiyo inadhibitiwa kabisa.

Bwana Khare pia aliwaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa na ripoti nyingine za visa vingine zaidi ya elfu moja vya ubakaji vilivyotendwa Kote nchini Congo mwaka jana.