Bobby Zamora avunjika, nje miezi minne

Bobby Zamora
Image caption Bobby Zamora

Fulham itamkosa Bobby Zamora kwa takriban miezi minne baada ya mshambuliaji huyo wa England kuvunjika mguu wakati timu yake ilipoishinda Wolves mabao 2-1 siku ya Jumamosi.

Zamora alitolewa nje kwa machela katika dakika ya 28 baada ya kuchezewa vibaya na Karl Henry.

Siku ya Ijumaa Zamora mwenye umri wa miaka 29, ambaye mwezi wa Agosti aliichezea England mechi yake ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Hungary, alisaini mkataba wa kuichezea Fulham kwa miaka mingine minne hadi mwaka 2014.

Kwa mujibu wa meneja wa Fulham. Mark Hughes, Zamora alivunjika mguu juu ya kiwiko na hatacheza kwa muda wa miezi minne.

Zamora alijiunga na Fulham akitokea West Ham mwezi wa Julai mwaka 2008 na baada ya kuwa na msimu mgumu, katika msimu wa 2009-10 alibadilika na aliweza kupachika mabao 19 yaliyoisaidia timu yake kufuzu kucheza Ligi ya Europa na Fulham ilimaliza katika nafasi ya 12 katika Ligi Kuu ya England.

Mshambuliaji huyo msimu huu wa ligi alianza vizuri baada ya kufunga katika mchezo dhidi ya Blackpool walipotoka sare ya mabao 2-2 kabla ya kupata matatizo ya msuli wa paja.

Kuumia huko kulimnyima nafasi ya kuiwakilisha England katika michezo ya kufuzu katika makundi ya mashindano ya Euro 2012 dhidi ya Bulgaria na Switzerland na amekuwa katika wasiwasi kama angeweza kucheza mechi dhidi ya Wolves.

Meneja wa Wolves Mick McCarthy amesisitiza timu yake haichezi mchezo wa rafu mbaya.