Kundi la LRA latishia Congo na Sudan

LRA
Image caption LRA

Viongozi wa mashirika ya dini na umma katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo , Sudan na Afrika ya kati wanasema kuwa jamii zao zinakabiliwa na vitisho vya kila siku kutoka kwa kundi la waasi la LRA.

Mkutano unaofanyika katika mji mkuu wa jimbo la Sudan ya kusini wa Equatoria, Yambio wametaka jumuia ya kimataifa ichukue hatua za haraka kusimamisha mauaji na utekaji nyara unaofanywa na LRA.

Akizungumza na BBC, askofu Eduardo Hiiboro Kassala ameyaelezea mateso yanayowafika kutokana na kundi la LRA kwa wakaazi wa eneo kubwa la Afrika ya kati kama makubwa mno.

Kundi la LRA lililoanzishwa nchini Uganda zaidi ya miaka 20 iliyopita kwa sasa linaendesha shughuli zake katika eneo lenye ukubwa wa kilomita elfu moja kuanzia mpaka wa Uganda, kupitia msitu mkubwa ulio kati ya Sudan ya kusini na Congo ya kaskazini hadi pori la Afrika ya kati.

Askofu amesema katika mkutano huo viongozi wa Congo walilielezea kundi la LRA kama linalozidi kuimarika na kupata ujasiri wa kushambulia vituo vya kijeshi badala ya vijiji vilivyojitenga kama tabia yao.

Kusini mwa Sudan nako waasi hao wameonyesha ujasiri ule ule kwa kushambulia eneo lililo kilomita tatu kutoka mji wa Yambio siku ya Jumamosi.

Askofu Hiiboro amesema kwa sasa watu laki moja na elfu ishirini wametapakaa katika eneo la Equatoria ya magharibi.

Tangu mwezi May watu elfu moja wameuawa na wengine wengi kutekwa nyara. Mkutano huo uliambiwa hadithi kama hiyo kutoka nchi nyingine pia.

Askofu Hiiboro ndiyo akauliza kwanini jumuia ya kimataifa inaruhusu vitendo hivi kuendelea.

Marekani inasema ina mipango ya kukabiliana na kundi hilo kwa kushirikiana na nchi za kanda ingawa juhudi zote za kukwamisha kundi la LRA zimeshindwa.