Marekani kufadhili kura ya maoni Sudan Kusini

uchaguzi Sudan Kusini

Marekani imesema inaongeza juhudi zake katika kuisaidia nchi ya Sudan kujiandaa kwa kura ya maoni katika Sudan Kusini.

Maafisa wa Marekani wamesema rais Barrack Obama atahudhuria mkutano wa ngazi ya juu wa viongozi utakaofanyika katika Umoja wa Mataifa na ambao utazingatia zaidi kura hiyo muhimu nchini Sudan.

Mkutano huo umepangwa kufanyika mwezi huu, kando ya mkutano wa kila mwaka wa baraza kuu la Umoja wa mataifa.

Wasiwasi kuhusu kura ya maoni inayopangwa kufanyika Januari mwakani unaongezeka nchini Marekani na katika Umoja wa Mataifa.

Hii ni kwa sababu matayarisho ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni yamechelewa, na ni machache yamefanyika kutatua mzozo ambao huenda ukalipuka iwapo eneo la Sudan Kusini litapiga kura ya kuamua uhuru wao.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema rais Obama ameamua kuhudhuria mkutano huo ili kulenga mtazamo wa kimataifa kuhusu suala hilo, katika miezi michache ijayo.

Awali, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hilary Clinton, aliitaja Sudan kama bomu linalotaka kulipuka.

''Hali katika jimbo la Darfur in ya hatari, ni ngumu na vile vile hakuna amani......lakini hali Kusini mwa Sudan ni kama bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote, na madhara yake yatakuwa makubwa zaidi'' . Bi Clinton alisema.

Waziri huyo wa mambo ya nje aheahidi kufanya kazi na washirika wao kuhakikisha kura hiyo ya maoni inafanyika kwa njia ya amani na kuisaidia Sudan Kusini kujitenga akidai ni matokeo ya kura hiyo ya maoni ni jambo a mbalo haliwezi kuzuilika.