Afghanistan wapinga kuchomwa Quran

Maelfu ya watu wameandamana nchini Afghanistan juu ya mipango, ambayo kwa sasa imeahirishwa, na kanisa dogo katika jimbo la Florida la kuchoma nakala za Quran.

Image caption Maandamano Pakistan

Watu watatu walipigwa risasi baada ya maandamno yaliyofanyika karibu na kituo cha majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya NATO kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo kuanza ghasia.

Rais Hamid Karzai alisema hatua hiyo ni kuufedhehesha Uislamu, huku Rais wa Indonesia akisema inatishia amani ya dunia.

Mchungaji Terry Jones amekiambia kipindi cha asubuhi cha televisheni cha Marekani kuwa alikuwa hana mpango wa kufanya hivyo.

Rais Barack Obama alionya kuwa itakuwa "bahati njema" kwa al-Qaeda katika kuwaajiri wafuasi wake, wakati waziri wa ulinzi Robert Gates alimwomba mchungaji huyo aahirishe hatua yake hiyo.

Maandamano mengi siku ya Ijumaa nchini Afghanistan yalifanywa baada ya waumini kutoka misikitini, baada ya swala ya Eid kufuatia kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Waandamanaji walichoma moto bendera ya Marekani na kupiga ukelele "vifo kwa Wakristo".

Mkuu wa polisi ameiambia BBC, watu 1,500 waliandamana kwenye mji mkuu wa Faizabad wa jimbo la Badakhshan.

Takriban watu wengine 150 walishiriki katika maandamano mengine mjini humo, wakirusha mawe na wakijaribu kupanda ukuta wa jengo la Nato ambapo ni makao makuu ya majeshi ya Wajerumani.