Jumanne haikuwa nzuri timu za England

Hekaheka za Ubingwa wa Ulaya
Image caption Patashika Manchester United na Rangers

Kurejea uwanjani kwa Wayne Rooney kulishindwa kuwa kichocheo cha Manchester United kushinda walipokwaa kisiki kigumu cha mpingo cha Rangers katika mechi ya kwanza ya Ubingwa wa Ulaya katika uwanja wa Old Trafford.

Timu hizo hazikufungana katika mchezo ambao Rangers walionekana dhahiri kuwakatisha tamaa washambuliaji wa United wasitikise nyavu za lango lao.

Rooney hakucheza mchezo wa ligi kuu ya England siku ya Jumamosi walipokutana na Everon huku kukiwa na tuhuma zilizogubika maisha yake binafsi na meneja wa United Sir Alex Ferguson kwa mshangao alibadilisha wachezaji 10 ambao hawakucheza dhidi ya Everton.

Manchester United kwa kumtumia zaidi Rooney walikuwa wakihaha uwanja mzima kutafuta bao huku vijana wa Walter Smith wakiwa wagumu kupitika.

Ferguson angalao alifarijika kwa kuweza kurejea uwanjani mlinzi wa kutumainiwa Rio Ferdinand aliyemudu dakika zote 90 tangu alipoumia goti wakati wa fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, lakini kuumia vibaya kiwiko cha mguu kwa mshambuliaji wa pembeni Antonia Valencia katika kipindi cha pili kulipeleka majonzi Old Trafford.

Nayo Tottenham ilianza mchakato wa Ubingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza kwa kuonesha kandanda safi ingawa walibanwa na kutoka sare ya mabao 2-2 na Werder Bremen.

Spurs walikuwa wa kwanza kutikisa lango la wenyeji wao baada ya mlinzi wa Bremen Petri Pasanen kujifunga mwenyewe kutokana na kushindwa kuzuia krosi ya Gareth Bale, kabla ya Peter Crouch kufunga bao zuri la pili kwa kichwa.

Lakini Bremen walijipanga upya na kuweza kupata bao la kwanza dakika mbili kabla mapumziko wakati Hugo Almeida alipofunga kwa kichwa kilichomzubaisha kipa Carlo Cudicini.

Matokeo hayo ina maana timu zote za kundi A zipo sawa baada ya Inter Milan nayo kwenda sare ya mabao 2-2 na klabu ya Uholanzi ya FC Twente.

Matokeo mengine kwa mechi za siku ya Jumanne za Ubingwa wa Ulaya:

Barcelona 5-1 Panathinaikos, Benfica 2-0 Hapoel Tel-Aviv, Bursaspor 0-4 Valencia na Copenhagen 1 Rubin Kazan 0.